Dawa ya kienyeji ya Covid-Organics yazidi kuwa maarufu Afrika

Dawa ya kienyeji kutoka Madagascar inayodaiwa inauwezo wa kutibu virusi vya covid-19, inazidi kupata umaarufu huku baadhi ya mataifa ya Afrika yakiendelea kuiagiza.

Ya hivi punde kununua dawa hiyo almaarufu Covid-Organics (CVO) ni Gambia ambayo tayari imepokea shehena ya kwanza kutoka Madagascar.

Shehena hiyo ilitumwa na Rais  Andry Rajoelina wa Madagascar, kulingana na taarifa iliyotolewa na ikulu ya Rais huko Gambia.

Taarifa hiyo ilisema shehena hiyo ni sehemu ya msaada kwa Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi – ECOWAS ili kusaidia katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa COVID-19.

Mataifa kadha ya Afrika yamepokea sampuli za dawa ya Covid-Organics (CVO) kutoka Madagascar mnamo wiki za hivi punde, huku baadhi ya mataifa hayo yakiitisha dawa zaidi.

Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania (kulia) akionja dawa ya kienyeji ya Covid-Organics kutoka Madagascar

Tanzania ni baadhi ya mataifa ambayo yameagiza dawa hiyo ya kienyeji katika juhudi ya kukabiliana na covid-19 nchini humo.

Rais  Andry Rajoelina wa Madagascar ambaye alizindua rasmi dawa hiyo mwezi uliopita, alisema inafaa kwa kutibu na kuzuia maambukizi ya COVID-19.

Rais Rajoelina aliitoa mfano wa watu 105 nchini mwake ambao wametibiwa na kupona kwa kutumia dawa hiyo.

Hayo yanajiri huku Shirika la Afya Duniani (WHO) likisema kuwa hadi sasa hakuna tiba ya virusi vya covid-19.  

Hata hivyo WHO inaziunga mkono dawa za kienyeji ambazo zimedhibitishwa kisayansi.