CORD Yatishia Kususia Uchaguzi Mkuu

Muungano wa CORD umeonya kwamba huenda ukalazimika kususia uchaguzi mkuu wa mwaka huu iwapo rais Uhuru Kenyatta ataidhinisha mswada tata wa marekabisho ya sheria ya uchaguzi. Kinara mwenza wa A�CORD Kalonzo Musyoka amedai kwamba wapinzani hawatashiriki kwenye uchaguzi ambao matokeo yake yatakuwa yameamuliwa awali. Kiongozi huyo wa chama cha Wiper aliyasema hayo katika kaunti ya Kajiado ambako alitoa wito kwa rais kudhihirisha uzalendo na kukataa sheria mpya ya uchaguzi iliyopitishwa hivi maajuzi.

Wapinzani wamewaita zaidi ya wawaniaji elfu-15 kwa mkutano Jumatano hii kujadili hatua za kuchukua baada ya chama cha Jubilee kutumia wingi wake bungeni kupitisha mswada tata wa marekebisho ya sheria hiyo ya uchaguzi. Hata hivyo viongozi wa mrengo wa Jubilee wamepuuzilia mbali madai ya wapinzani wakisema vitisho hivyo ni vitendo vya woga.