Cord Walaumu Jubilee Kwa Ufisadi Nchini

Viongozi wa mrengo wa CORD wameishutumu serikali kwa madai ya kuzitenga baadhi ya jamii za humu nchini. Wakiongea wakati wa dhifa ya heshima kwa kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka ambaye amependekezwa kwa tuzo la mtu mashuhuri barani Afrika, viongozi hao waliilaumu serikali ya Jubilee kwa kuchangia umaskini unaokithiri hapa nchini kwa kutochukua hatua dhidi ya ufisadi. Na licha ya serikali kujiondolea lawama dhidi ya ufisadi huku ikizilaumu asasi zinazopasa kupambana na ufisadi kwa kuwa kizingiti kwa vita hivyo, mrengo wa upinzani unasisitiza kuwa utawala wa Jubilee unapaswa kuwajibikia visa hivyo. Viongozi hao walisema serikali haionekani kuwa na azma ya kuchukua hatua zozote dhidi ya visa vya ufisadi. Aidha walisema serikali imeyatenga baadhi ya maeneo ya hapa nchini huku wakihimiza umuhimu wa kudumisha amani na utangamo miongoni mwa Wakenya. Alisema mfumo wa ugatuzi ndiyo njia pekee ya kuhakikisha ugavi sawa wa rasilimali na kuzuia upendeleo.