CORD Yamtaka Tobiko Kumfungulia Duale Mashtaka

Mrengo wa CORD umeelekea mahakamani kumshinikiza mkurugenzi wa mashtaka ya umma, Keriako Tobiko kumfungulia mashtaka kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa, Aden Duale. CORD wamedai kuwa matamshi ya mbunge huyo wa Garissa Mjini dhidi ya jaji George Odunga yanashusha hadhi ya mahakama na kuhujumu utekelezaji haki. Kupitia wakili wake Apolo Mboya, muungano wa CORD umesema matamshi ya Duale yalifedhehesha mamlaka ya idara ya mahakama na pia kuingilia shughuli za idara hiyo na utekelezaji haki. Kesi hiyo itatajwa tarehe 24 mwezi huu kwa maagizo zaidi. Kwingineko ,mbunge wa Kabete, Ferdinand Waititu, amewasilisha kesi mahakamani kuzuia utekelezaji mkataba wa maelewano ambao umeafikiwa kati ya serikali ya kaunti ya Kiambu na halmashauri ya ukusanyaji ushuru hapa nchini-KRA. Waititu anapinga makubaliano hayo akisema yaliafikiwa pasipo kushirikisha, kuelemisha wala kuhamasishaA� A�umma. Kupitia kibali cha dharura mbunge huyo pia anadai kwamba makubaliano hayo hayakuidhinishwa na bunge la kaunti ya Kiambu.