Cocaine kilo 2.5 yenye thamani ya milioni 8 yanaswa Jomo Kenyetta Airport

Maafisa wa halmashauri ya ukusanyaji ushuru hapa nchini wamenasa dawa za kulevya aina ya Cocaine za uzani wa kilo 2.5 za thamani ya shilingi milioni 8 katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta. Juhudi za mlanguzi wa dawa za kulevya raia wa Venezuela za kulangua dawa hizo hapa nchini zilitibuliwa wakati wa siku kuu ya Krismasi wakati wa shughuli ya kawaida ya ukaguzi wa abiria katika uwanja huo.Akiongea alipothibitisha kisa hicho ,kamishna wa maswala ya forodha na udhibiti wa mipakani Julius Musyoki alisema mihadarati hiyo ilikuwa imefichwa upande wa chini ya mkoba wa mlanguzi huyo.Mlanguzi huo aliyetambulishwa kama Medina Paez Maria Artmelis alikuwa amewasili katika uwanja huo wa ndege kutoka Addis Ababa kwa ndege ya shirika la ndege la Ethiopia akiwa na cheti cha visa cha utalii. Kunaswa kwa mihadarati hiyo na maafisa wa KRA kwa ushirikiano na kundi la usalama la mashirika mbali mbali linalojumuisha ujasusi wa visa vya uhalifu , huduma ya taifa ya polisi , idara ya kitaifa ya ujasusi na halmashauri ya viwanja vya ndege hapa nchini ni sehemu ya mkakati wa usalama uliowekwa wakati huu wa msimu wa krismasi. Mihadarati hiyo imekabidhiwa kitengo cha polisi wa kukabiliana na ulanguzi wa dawa za kulevya kwa uchunguzi zaidi huku mshukiwa akitarajiwa kufikishwa mahakamani leo.