Chuo Kikuu Cha Nairobi Chasitisha Masomo Ya Wanafunzi 139 Zaidi

Chuo kikuu cha Nairobi kimewasimamisha kwa muda wanafunzi 139 zaidi kuendelea na masomo yao hivyo kufikisha 201 jumla ya wanafunzi waliosimamishwa katika siku mbili zilizopita. Hapo jana wanafunzi 62 walisimamishwa kuendelea na masomo yao kufuatia ghasia zilizokumba chuo hicho kufuatia uchaguzi wa viongozi wa wanafunzi uliozozaniwa. Naibu chansela Profesa Peter Mbithi alisema chuo hicho kimeanzisha utaratibu wa kinidhamu dhidi ya wanafunzi hao kwa kushiriki kwenye ghasia hizo na uharibifu wa mali. Profesa Mbithi alisema wanafunzi walioathiriwa wanaweza kuchukua barua zao za kusimamishwa masomo kutoka kwa afisi ya msajili. Miongoni mwa wanafunzi waliochukuliwa hatua ya nidhamu ni Mike Jacobs, aliyepinga matokeo ya uchaguzi huo baada ya kushindwa kwenye uchaguzi wa mwenyekiti wa chama cha wanafunzi-SONU na Paul Ongili al-maarufu Babu Owino. Jumatatu iliyopita, wanafunzi wa chuo kikuu cha Nairobi waliandamana wakilalamikia kuchaguliwa tena kwa Owino kuwa mwenyekiti wa chama cha SONU kwa mara ya nne mfululizo wakisema wasimamizi wa chuo hicho walishiriki kwenye wizi wa kura ili kumwezesha Owino kuchukua uongozi. Wanafunzi hao waliteketeza afisi za chama hicho mbali na kufunga barabara za University Way na Uhuru Highway kabla ya kutawanywa na maafisa wa polisi.