Chuo Kikuu Cha Nairobi Chafungwa Kufuatia Maandamano Za Ghasia

Chuo kikuu cha Nairobi-UON kimefungwa mara moja kufuatia siku tatu za maandamano ya ghasia kuhusu uchaguzi wa chama cha wanafunzi uliopingwa. Katika taarifa, baraza la chuo hicho na naibu wa Chancellor Profesa Peter Mbithi aliwaagiza wanafunzi waondoke katika mabewa yote ya chuo hicho kabla ya saa kumi na moja jana jioni. Alisema uamuzi wa kukifunga chuo hicho ulifikiwa kufuatia kuendelea kutatizwa kwa shughuli za kawaida za chuo hicho na makundi ya wanafunzi waliotokwa na nidhamu. Hatua hiyo iliyotangazwa baada ya mkutano maalum wa baraza la chuo kikuu hicho inahusu mabewa yote ya chuo kikuu cha Nairobi, na ni pigo kwa wanafunzi waliojiandaa kufanya mitihani yao ya muhula wa masomo kuanzia Jumatatu wiki ijayo. Wanafunzi hao wamekuwa wakifanya ghasia tangu Jumamosi kupinga kuchaguliwa tena kwa Babu Owino kuwa mwenyekiti wa chama cha wanafunzi wa chuo kikuu cha Nairobi (SONU). Ghasia hizo zilizidi jana wakati wanafunzi walipoteketeza ofisi za SONU zilizopo kwenye barabara ya University Way. Chuo kikuu hicho kimefungwa huku polisi wakianzisha uchunguzi wa video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii inayoonyesha polisi wakiwacharaza viboko makundi ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Nairobi.