Cheyech kuongoza wanariadha wa Kenya katika mbio za nusu marathoni za jumuiya ya madola

Aliyekuwa bingwa wa mbio za marathoni za Jumuiya ya madola Filomena Cheyech  atawaongoza wanariadha wa humu nchini kushiriki katika makala ya kwanza ya mbio za nusu marathoni za jumuiya ya madola zitakazoandaliwa jumapili hii jijini Cardiff, Wales.

Kikosi cha Kenya kinajumuisha bingwa wa mbio za nusu marathoni za Cardiff  mwaka jana John Lotiang, Joseph Nzioki  na Daniel Muteti. Wanariadha hao wa humu nchini wanatarajia ukinzani mkali kutoka wanariadha wa Uganda.

Kikosi cha Uganda kinajumuisha aliyekuwa bingwa wa  dunia wa mbio za milimani Fred Musobu, bingwa wa mwaka jana wa mbio za mita elfu 10 nchini Uganda Timothy Toroitich, Felix Chemonges na  Vitalis Kwemoi.

Zaidi ya mataifa 50  yanatarajiwa kushiriki katika mashindano hayo yakiwemo Australia, Canada, Afrika Kusini na Nigeria. Mashindano hayo yanayaleta pamoja mataifa yaliyokuwa chini ya ukoloni wa Uingereza.