Chebukati awataka maafisa wa IEBC waliochangia ubatilishaji wa uchaguzi kujiuzulu

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi na mipaka, IEBC, Wafula Chebukati, amewataka maafisa wa tume hiyo waliohusishwa na makosa yaliyosababisha kubatilishwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais mwezi wa nane kujiuzulu kabla ya marudio ya uchaguzi huo. Kwenye kikao na wanahabari kwenye ukumbi wa Bomas, Chebukati alisema hata ingawa tume hiyo imejiandaa kwa marudio ya uchaguzi wa urais juma lijalo, juhudi za kuhakikisha uchaguzi huo utakuwa huru, wa haki na kuaminika zinahujumiwa na baadhi ya makamishna wa tume hiyo. Chebukati aliwatahadharisha viongozi wa mirengo ya NASA na Jubilee kuwa macho ya jamii ya kimataifa yameelekezwa humu nchini na akahimiza mashauriano kati ya tume hiyo na viongozi wakuu wa kisiasa. Chebukati aliwaonya viongozi hao dhidi ya kuvuruga utendakazi wa tume hiyo akisema hatakubali kuketi kitako wakati wanasiasa wakisababisha vurugu humu nchini. Hata hivyo Chebukati alisema hana nia ya kujiuzulu kama mwenyekiti wa tume hiyo kwa kuwa amejitolea kuhakikisha marudio ya uchaguzi wa urais ni ya kuaminika.