IEBC Yasisitiza ndiyo ina mamlaka ya kutangaza matokeo ya uchaguzi mkuu

Mwenyekiti wa Tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) Wafula Chebukati ameviambia vyama vya kisiasa kwamba ni tume hiyo pekee ndiyo iliyo na jukumu la kutangaza matokeo ya uchaguzi utakaofanyika Agosti 8. Katika taarifa, Chebukati alisema tume hiyo inachukulia kwa umuhimu taarufa za baadhi ya vyombo vya habari zinazosema kuwa muungano wa NASA utatangaza matokeo yake sambamba na tume hiyo. Mkuu huyo wa IEBC alisema ni tume hiyo pekee ndiyo inayoruhusiwa chini ya sheria kuhesabu, kuorodhesha , kukusanya na kutangaza matokeo ya uchaguzi. Alisema taasisi nyingine vikiwemo vyama vya kisiasa zitaweza kupata matokeo katika utaratibu uliowekwa na tume hiyo. Pia Chebukati aliwahakikishia washiriki wote kwamba itachukua hatua zote kuhakikisha kwamba matokeo ya uchaguzi huo yanadhihirisha matarajio ya watu. Akikariri kujitolea kwa tume hiyo kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unafanyika kwa njia huru na ya haki na wa kuaminika Chebukati alisema tume hiyo aidha imeandaa utaratibu wa usimamizi wa matokeo unaopatikana kwenye tovuti yake unaofafanua taratibu itakayofuatwa na tume hiyo katika kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika uchaguzi huo.