Chebukati apuuzilia mbali madai kuwa akutana usiku na viongozi wa NASA

Mwenyekiti wa tume ya IEBC, Wafula Chebukati amepuuzilia mbali madai kuwa amekuwa akikutana usiku na viongozi wa muungano wa NASA. Kupitia ujumbe wake kwenye kitandazi cha twitter, Chebukati alisema madai hayo ni ya uongo, hayana msingi na kamwe hayatabadili azma ya tume hiyo ya kuandaa marudio ya uchaguzi wa urais kwa njia ya haki. Chebukati aliwataka wale walio na ushahidi kuhusu mikutano hiyo ya usiku na mahali ilikofanyika kufafanua hadharani. Kwingineko, tume ya IEBC inaendelea na vikao vyake mjini Naivasha kujadili mbinu za kufanikisha marudio ya uchaguzi wa urais mwezi ujao. Tume hiyo ambayo imekuwa ikiangaziwa baada ya kubitilishwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais na migogoro ya ndani kwa ndani inapania kutumia kikao hicho kutatua changamoto hizo kabla ya uchaguzi huo wa tarehe-17 mwezi Oktoba.