Chama cha Zanu-PF cha Zimbabwe chabuni mbinu ya kuwashawishi wanachama wapya

Chama tawala nchini Zimbabwe-Zanu-PF kimebuni mbinu mpya ya kuwashawishi wanachama wapya kwa kuwapa kadi za uwanachama ambazo pia zinaweza kutumiwa kama kadi za kutoa pesa kwenye benki. Mbinu hiyo huenda ikavutia wanachama zaidi kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka-2018. Maafisa wa chama cha Zanu-PF wamesema maelezo kwenye kadi hizo yatanakiliwa kwenye mfumo wa benki ya kitaifa ya akiba kwani kadi hizo zitakuwa na nambari ya akaunti ya benki ya mwanachama husika. Hata hivyo wakazi wengi wa maeneo ya mashambani nchini Zimbabwe hawana akaunti za benki ambazo kwa kawaida hutumiwa kwa malipo ya mishahara ya wafanyikazi. Aidha, mbinu hiyo itakisaidia chama hicho tawala kuimarisha ukusanyaji wa ada za uwanachama ambazo zitakatwa moja kwa moja kutoka akaunti za benki za wanachama hao.