Chama cha wauguzi chataka suluhisho la kudumu kwa matakwa yao.

Chama cha kitaifa cha wauguzi kimesema kingali kinashauriana na wizara ya afya na baraza la magavana kwa lengo la kutafuta suluhisho la kudumu kwa matakwa yao. Mgomo huo ambao jana uliingia siku ya 74 ulitokana na hatua ya baraza la magavana kukataa kutia saini na kutekeleza makubaliano yaliyoafikiwa mapema mwaka huu. Kaimu katibu mkuu wa chama hicho Morris Opetu sasa anatoa wito kwa rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati mzozo huo. Opetu kadhalika aliwahakikishia wauguzi kwamba chama hicho kinashauriana na tume ya kutathmini viwango vya mishahara ya watumishi wa umma ili kuhakikisha wauguzi pia wananufaika na viwango vipya vya mishahara na utathmini wa mpangilio wa kazi kwenye utumishi wa umma uliofanywa na tume hiyo. Wiki kadhaa kabla ya uchaguzi mkuu, maafisa wa chama hicho waliondoka kwenye mkutano na baraza la magavana wakililaumu baraza hilo kwa kuto-kuwa na ajenda ya kumaliza mgomo huo. Huduma katika hospitali nyingi za umma kote nchini zingali zimekwama kutokana na mgomo huo.