Chama Cha ODM Chaapa Kudumisha Kiti Cha Gavana Nairobi

Chama cha ODM kimesema kitafanya kila juhudi kudumisha kiti cha gavana cha Nairobi katika uchaguzi mkuu ujao. Wakati huo huo, baadhi ya wanachama wa ODM wamemuidhinisha naibu mkuu wa chama hicho, aliye pia gavana wa Mombasa, Hassan Joho, kuwa mgombeaji wake wa urais mwaka 2022. Chama hicho kilizindua msururu wa mikutano yake ya hadhara katika kaunti ya Nairobi kwa maonyesho ya barabarani ambayo kilele chake kilikuwa mkutano wa kisiasa katika uwanja wa Masinde Muliro, eneo bunge la Mathare kwa uongozi wa Joho na mwenzake wa Nairobi, dakta Evans Kidero. Stephen Kariuki ambaye ni mbunge wa Mathare amekuwa mwanachama wa ODM kabla ya kuhamia mrengo wa Jubilee. A�Aidha, Joho alitumia fursa hiyo kutangaza azma yake ya kuwania urais mwaka 2022. Naibu wa Rais William Ruto, pia anatarajiwa kuwania kiti hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022. Hata hivyo, punde baada ya kukamilika kwa mkutano huo, ghasia zilizuka, ambapo mwenye gari moja la Pick-Up alikadiria hasara aliyopata, baada ya baadhi ya wafuasi wa chama cha ODM kuliteketeza gari lake kwa madai kwamba lilikuwa limewagonga watu kadhaa. Dereva wa gari hilo alilazimika kukimbilia usalama wake baada ya kukabiliwa na umati uliokuwa na hasira. Ilibidi lori la polisi lenye mabomba ya kunyunyiza maji lililokuwa likishika doria mahala hapo kuingilia kati kuuzima moto huo lakini gari hilo lilikuwa limeteketea kabisa.