Chama cha madaktari wakanusha kuwepo kwa mgomo

Katibu mkuu wa chama cha madaktari na madaktari wa meno (KMPDU) Dr. Ouma Oluga amekanusha taarifa kwamba madaktari wamegoma kufuatia kutolipwa kwa mishahara na marupurupu yao kwa miezi mitatu waliyokuwa wamegoma. Oluga alisema madaktari walikuwa wakilalamika kwa kutolipwa mishahara na marupurupu yao akiongeza kwamba kaunti zote zimeathirika. Dr. Oluga aliliambia shirika la utangazaji la KBC kwa njia ya simu kwamba chama hicho kiko makini kufuatilia matukio hayo na kitatoa ushauri kuhusu hatua itakayofuata ikichukuliwa kwamba madaktari wamevunjwa moyo tangu baraza la magavana lilipokataa kuwalipa kwa siku 100 walizokuwa wamegoma.
Katika kaunti ya Busia gavana wa kaunti hiyo Sospeter Ojaamong amesema kwamba madaktari hawatalipwa kwa siku walizokosa kufika kazini kama ilivyoagizwa na serikali na baraza la magavana. Wakati huo huo madaktari na wauguzi katika hospitali ya kaunti ya Busia wametisha kugoma wakitaka wapate huduma bora za usafi. Hiyo imetokea huku wafanyakazi walioajiriwa na serikali ya kuanti hiyo kudumisha usafi kwenye vyoo kugoma wakiilaumu serikali hiyo ya kaunti kwa kushindwa kuwalipa malimbikizi ya mishahara ya miezi mitatu.