Chama cha madaktari kimepewa siku tano kutatua mgomo wa madaktari

Jopo la majaji watatu wa mahakama ya rufani limewapa wapatanishi na chama cha madaktari na wataalamu wa meno-KMPDU siku tano zaidi ili kuendelea na mashauri ya kutatua mgomo wa madaktari. Wapatanishi kwenye harakati hizo za kusitisha mgomo wa madaktari ambao umedumu kwa siku-88 wakiongozwa na tume ya kitaifa ya kutetea haki za binadamu-KNCHR na chama cha wanasheria hapa nchini-LSK leo waliwasilisha ripoti kuhusu mashauriano hayo, lakini majaji wa mahakama ya rufani Martha Koome, GBM Kariuki na Jamila Mohammed walisema itachukuliwa kuwa ripoti ya muda tu. Maafisa wa chama hicho cha madaktari waliachiliwa huru majuma mawili yaliyopita ili kuwawezesha kuendelea na mashauriano kuhusu mkataba wa pamoja wa mwaka 2013 unaodaiwa kutiwa sahihi na aliyekuwa katibu katika wizara ya afya wakati huo. Wapatanishi hao watarejea mahakamani jumanne ijayo.