Bunge limeanza kuwasaili waliopendekezwa kuwa mawaziri

Bunge jana lilianza kuwasaili watu tisa waliopendekezwa kuwa mawaziri huku aliyependekezwa kuwa waziri wa utumishi wa umma Profesa Margaret Kobia akiwa wa kwanza kuhojiwa. Aliyekuwa gavana wa Meru, Peter Munya, alikuwa wa mwisho kusailiwa kwenye siku ya kwanza ya usaili. Munya alipendekezwa kuwa waziri wa utangamano wa Afrika mashariki. Wengine waliofika mbele ya kamati ya usaili iliyoongozwa na spika wa bunge la taifa Justin Muturi ni aliyekuwa seneta wa Turkana, John Munyes, ambaye amependekezwa kuwa waziri wa bidhaa za petroli na uchimbaji madini, Monica Juma ambaye amependekezwa kuwa waziri wa mashauri ya kigeni na biashara ya kimataifa na mwanahabari Faridah Karoney aliyependekezwa kuwa waziri wa ardhi na nyumba. Wakati wa usaili huo Profesa Kobia alisema kwamba wakati wa muda ambao atahudumu, ataratibu mfumo wa kuwapandisha vyeo watumishi wa umma ili kuwapa motisha na uadilifu wa kuhudumia umma.

Naye Bi. Juma amefafanua kwamba maongozi ya kigeni ya nchi hii yanazingatia sera za bara Afrika ambazo zinajumuisha uzingativu maslahi ya mataifa ya eneo la mashariki na upembe wa Afrika.