Bodi ya Kenyatta yawarejesha maafisa wanne wa matibabu waliohusika katika mchanganyiko wa upasuaji kazini

Bodi ya hospitali kuu ya  kitaifa ya Kenyatta imewarejesha kazini maafisa wanne wa matibabu waliohusika katika mkanganyiko wa upasuaji wa kichwa katika juhudi za kutuliza hali na kubuni mazingra bora ya uchunguzi. Mwenyekiti wa bodi hiyo Mark Bor ameelezea hatua hiyo kuwa ishara ya nia njema inayolenga kukomesha mahangaiko ya wagonjwa wengi na kushughulikia malalamishi ya madaktari .Uamuzi huo uliafikiwa baada ya  mkutano kati ya waziri wa afya Sicily Kariuki, bodi ya hospitali hiyo na bodi ya wahudumu wa matibabu na wataalam wa meno hapa

Mwenyekiti wa bodi ya wahudumu wa matibabu na wataalam wa meno hapa nchini  Prof George Magoha amesema bodi hiyo itazindua uchunguzi kuhusiana na kisa hicho katika muda wa siku saba zijazo.

Waziri wa afya Sicily Kariuki amesema  anatarajia kupokea ripoti za uchunguzi kutoka kwa hospitali kuu ya kitaifa ya Kenyatta na bodi za madaktari siku ya Ijumaa ili hatua zaidi ichukuliwe. Wagonjwa walioathirika na mkanganyiko huo waliruhusiwa kuondoka hospitalini siku ya Jumatano . Samuel Kimani na  John Nderitu waliruhusiwa kuondoka hospitalini huku madaktari wakitangaza kuwa wako katika hali dhabiti na wataendelea kupata nafuu wakiwa nyumbani.