Bingwa wa mbio za marathoni za London Mary Keitani ashinda taji ya Great North Run

Bingwa wa mbio za marathoni za London Mary Keitany  alishinda taji ya mbio za  Great North Run kwa mara ya tatu baada ya kutumia muda wa saa 1 dakika 05 na sekunde 59 nchini Uingereza.  Keitany  ambaye pia alishinda taji ya mbio za marathoni za New York mwaka jana alizikamilisha mbio hizo za kilomita 21, dakika moja na sekunde 45, mbele ya mwenzake Vivian Cheruiyot, aliyeshinda mbio hizo mwaka jana. Caroline Kipkirui, alimaliza wa tatu kwa muda wa saa 1 dakika 09 na sekunde 52 ilihali  Magdalyne Masai  pia wa humu nchini akakamilisha mbio hizo katika nafasi ya nne.  Taji ya wanaume ilitwaliwa na Mo Farah wa Uingereza aliyeshinda taji hiyo kwa mara ya nne mfululizo.   Farah, ambaye ni bingwa mara nne wa Olimpiki, alimpiku Jake Robertson  wa New Zealand katika awamu ya mwisho na kushinda mbio hizo kwa muda wa saa 1 na sekunde sita.  Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 34 ni mwanariadha wa kwanza mwenye umri zaidi ya 30 kushinda mbio hizo za Great North Run mara nne mfululizo. Mbio hizo za kilomita 21 zilizoanzia Newcastle  na kukamilika mjini South Shields   ziliwavutia jumla ya wanariadha  12,000  kutoka kote duniani.