Bi. Melania Trump aanza rasmi ziara Kenya

Mkewe  Rais wa Marekani Bi. Melania Trump ambaye yuko humu nchini kwa ziara ya ki-serikali ya siku mbili, alianza shughuli zake leo asubuhi kwa kutembelea wakfu wa kuhifadhi wanyama pori wa David Sheldrick. Melania aliandamana na mwenyeji wake, Mama wa taifa Bi. Margaret Kenyatta.

Wakfu huo wa David Sheldrick ni mojawapo ya taasisi za kwanza za kuhifadhi wanyama na kutunza mazingira katika eneo la  Afrika Mashariki. Bi. Trump anatarajiwa kupigia debe mradi wake wa Be Best”, ambao malengo yake ni sawa na yale ya mardi wa Bi. Margaret Kenyatta wa “Beyond Zero”.

Wake hao wa Ma-Rais wanatarajiwa kushirikiana juu ya mpango utakaohakikisha kwamba majukumu ya miardi hiyo miwili yanaenda bega kwa bega. Baadaye hii leo; Melania na mwenyeji wake wanatarajiwa kufika katika ukumbi wa Kenya National Theatre ambako watatumbuizwa kwa michezo na ngoma za utamaduni wa humu nchini.

Polisi tayari wamefunga barabara ya Harry Thuku, kabla ya kuwasili kwa Bi. Melania Trump katika ukumbi huo wa  Kenya National Theatre”. Melania aliwasili humu nchini jana jioni, baada ya kukamilisha ziara yake nchini Ghana na Malawi. Hii ndiyo ziara yake ya kwanza barani Afrika bila kuandamana na Mumewe. Anatarajiwa kukamilisha ziara yake ya bara Afrika huko Misri.