Bernard Kiala ajiondoa kwenye kinyanganyiro cha ugavana Machakos

Naibu gavana wa Machakos, Bernard Kiala, aliyekuwa akiwania wadhifa wa ugavana akiwa mgombeaji huru, amejiondoa kwenye kinyanganyiro cha uchaguzi mkuu wa tarehe 8 mwezi ujao. Akiongea na wanahabari ,A� Kiala alisema alichukua hatua hiyo baada ya kushauriana na wazee na viongozi wa jamii ya Wakamba. Aidha alisema hatua hiyo inanuia kuhakikisha udhabiti wa muungano wa NASA katika uchaguzi mkuu ujao. Kiala, aliyeandamana na Bi. Evelyn Mutula, hata hivyo alisema hakujiondoa kwa manufaa ya mgombeaji yeyote. Wakati huo huo, mgombeaji kiti cha ugavana wa Machakos kwa tiketi ya muungano wa NASA, Wavinya Ndeti amesifu hatua hiyo ya Kiala ya kujiondoa katika kinyanganyiro hicho, siku nane kabla ya uchaguzi mkuu. Kwenye taarifa, Ndeti alisema anachukulia hatua hiyo kwa umuhimu, akisema inaonyesha kwamba Kiala amejitolea kushirikiana na kuhakikisha muungano wa NASA umeshinda katika uchaguzi mkuu ujao. Aliwahakikishia wakazi wa kaunti ya Machakos kwamba viongoziA� wote wa NASA katika eneo hilo watafanya kazi kwa pamoja wakichaguliwa katika uchaguzi ujao.A� Kiala alihama chama cha Kalonzo baada ya kushindwa na Wavinya Ndeti katika uteuzi wa chama hapo mwezi Aprili, lakini alipinga matokeo mara kadhaa lakini alishindwa pia.