BBC Yawekeza dolla milioni 10 Kenya

Shirika la utangazaji la Uingereza-(BBC), litawekeza karibu dolla A�million-10 za kimarekani katika ujenzi wa studio za kisasa za uandishi wa habari humu nchini ambazo zitabuni nafasi mpya 250 za ajira. Hayo yamesemwa leo na mhariri mmoja mkuu wa shirika hilo kwenye aarifa kwa Rais Uhuru Kenyatta. Solomon Mugera ambaye ni mhariri mkuu wa habari alisema kwamba uwekezaji huo utatoa mazoezi ya kikazi na mpango wa kuwashauri wanahabari chipukizi, na pia waelekezi wa kidijitali na kiufundi. Kwa mujibu wa aarifa hiyo kutoka Nairobi, shirika la BBC litashirikiana na watangazaji wa humu nchini na pia kampuni za kibinafsi za utayarishaji vipindi katika maandalizi ya vipindi vya humu nchini na pia kanda hii, vinavyotosheleza mahitaji ya watu wa tabaka mbali mbali, vikiwemo vya maswala ya biashara na afya. Shirika hilo la BBC pia linapanga kuzindua idhaa nyingine 6 za lugha mbali mbali A�zikiwemo lugha za Amharic, Afaan Oromo na Tigrinya ambazo zitapeperushwa kutoka Nairobi ili kuhudumia watu wa Ethiopia na Eritrea. Tayari shirika la BBC limekuwa lipeperusha matangazo na vipindi vyake katika lugha za Kiswahili na Somali kutoka Studio zake za Nairobi. Idhaa nyingine tatu katika lugha za Yoruba, Igbo na Pidgin zitapeperusha vipindi na matangazo yake kutoka Lagos, Nigeria. Rais Kenyatta alilipongeza shirika hilo la BBC kutokana na uwekezaji huo mpya nchini Kenya, akisema kwamba nchi hii inafahamika kwa maadili yake ya democrasi, yanayotilia maanani uhuru wa vyombo vya habari, talanta na ujuzi katika maswala ya uandishi na sanaa, na pia miundo msingi ya teknolojia ya habari isiyo na kifani katika bara hili la Afrika.