Barnaby Joyce hapaswi kushikilia wadhifa wa umma nchini Australia

Serikali ya New Zealand imethibitisha kuwa naibu waziri mkuu wa Australia,A� Barnaby Joyce ana uraia wa nchi mbili na hivyo hapaswi kushikilia wadhifa wa umma chini ya katiba ya Australia. Joyce alidokeza mapema mwaka huu kwamba huenda yeye ni raia wa New Zealand kutokana na uzao wake lakini amesema atawasilisha swala hilo kwenye mahakama kuu nchini humo. Serikali ya waziri mkuu, Malcolm Turnbull inakabiliwa na hatari ya kubanduliwa mamlakani iwapo itabainika kuwa Joyce hapaswi kushikilia wadhifa wake. Waziri wa maswala ya ndani nchini New Zealand, Peter Dunne alithibitisha kuwa chini ya katiba ya nchi hiyo, mtoto ambaye mzazi wake ni raia wa New Zealand anapata uraia wa nchi hiyo moja kwa moja. Hata hivyo, Joyce aliliambia bunge la nchi hiyo kwamba alishauriwa kuwa hajakaidi sheria yoyote. Joyce atasalia kuwa naibu waziri mkuu wa Australia. Joyce ni mwanasiasa wa hivi punde nchini Australia kukumbwa na utata kuhusu uraia wake.