Baraza la magavana latoa wito wa kuharakishwa kwa mswada wa mipaka ya kaunti

Baraza la magavana limetoa wito wa kuharakishwa kwa mswada wa mipaka ya kaunti wa mwaka 2019 ambao kwasasa umewasilishwa katika bunge seneti kuhakikisha kuwa mizozo ya kimipaka inasuluhishwa bila ya kuelekea mahakamani . Akihutubia warsha ya bunge la seneti la uhamasishaji kuhusu utangamano mwenyekiti wa baraza hilo Josephat Nanok alisema kuwa kupitishwa kwa mswada huo kutatoa muongozo wa kusuluhisha mizozo katika takriban kaunti 33 zinazokumbwa na mizozo ya kimipaka . Mizozo hiyo inayohusisha zaidi ya nusu ya kaunti zote 47 imetishia kutatiza utekelezaji wa amani wa ugatuzi . Sheria hiyo iliyopendekezwa inanuia kumpa rais mamlaka ya kubuni kamati za upatanishi kupitia maamuzi ya bunge la seneti kutatua mizozo kabla ya kuzuka kwa makabiliano .