Baraza la Magavana lasisitiza kufutwa kazi kwa wauguzi wanaogoma

Baraza la Magavana nchini limesisitiza kwamba wauguzi ambao bado wanagoma watafutwa kazi na seriakli za kaunti zao mbali mbali. Mwenyekiti  wa baraza la Ma-Gavana Joseph Nanok alisema baraza hilo limewaagiza Magavana kuwachukulia hatua  wauguzi wanaogoma kwani mgomo huo ulitangazwa na mahakama kuwa haramu. Hayo yamejiri huku chama cha kitaifa cha wauguzi (KNUN),  kikisisitiza kwamba wanachama wake wataendelea na mgomo. Nanok alisema kwamba serikali za kaunti ziko huru kutangaza kuwa wazi nafasi za wauguzi wanaogoma na kuajiri wauguzi wapya mahala pa wale waliokosa kufika kazini kufikia tarehe 8 Septemba. Alisema kwamba hakuna fursa nyingine ya mazungumzo  hadi wauguzi wanaogoma watakaporejea kazini la sivyo watafutwa kazi. Nanok alikuwa akiongea huko  leo mjini Nyahururu ambako alikwenda kuifariji familia ya gavana wa Laikipia Ndiritu Muriithi aliyempoteza Mamake Mumbi Muriithi mwishoni mwa  juma.