Bajeti 2017/2018 itawasilishwa leo miezi miwili mapema kuliko muda ulioratibiwa

Taarifa ya maongozi ya bajeti kwa kipindi cha mwaka 2017/2018 itawasilishwa leo miezi miwili mapema kuliko muda ulioratibiwa. Hatua hii inanuiwa kutoa fursa kwa wabunge kupitisha miswada muhimu kabla ya kwenda likizoni. Bajeti ya mwaka huu ni tofauti na zile zilizotangulia kwani haitasomwa Alhamisi ya pili ya mwezi Juni kama ilivyoratibishwa kwenye katiba. Kabla ya kusomwa kwa taarifa ya maongozi ya bajeti ya trilioni 2.62 hivi leo, wataalam wa kiuchumi wanasema kwamba serikali huenda isiwe na utathmini kamili wa matumizi na ushuru uliokusanywa kwa kipindi cha sasa cha matumizi ya fedha kama vile ukusanyaji ushuru, nakisi ya bajeti na utathmini wa matumizi ya fedha hali ambayo itasababisha kurekebishwa kwa matumizi ya fedha serikalini na ukusanyaji ushuru katika kipindi kijacho cha matumizi ya fedha za serikali. Kwa kiwango kikubwa bajeti iliyopendekezwa itafadhiliwa kwa ushuru wa mapato huku halmashauri ya ukusanyaji ushuru ikipewa lengo la kukusanya ushuru wa kiasi cha shilingi trilioni 1.7.