Babu Owino agoja kufahama ikiwa ataachiliwa kutoka korokoroni

Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino, leo alasiri atafahama ikiwa ataachiliwa kutoka korokoroni baada ya kukabiliwa na mashtaka mapya. Babu ambaye amechaguliwa mbunge kwa mara ya kwanza anadaiwaA� kumdhulumu mpiga kura wakati wa uchaguzi mkuu wa agosti-8. Owino alikanusha shtaka jingine la kukaidi sheria za uchaguzi wakati wa kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu katika eneobunge lake alipofikishwa mahakamani, Kibera. Owino alikamatwa tena jana, dakika chache tu baada ya kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi nusu milioni kwa mashtaka ya kumtusi rais na kutoa matamshi ya uchochezi. Alizuiliwa katika kituo cha polisi cha Pangani. Upinzani umekashfu kukamatwa tena kwa Babu Owino ukidai serikali inatumia mbinu za mateso na dhuluma. Mkurugenzi wa mashtaka ya umma ameagiza Owino achunguzwa kubaini ikiwa alikiuka sura ya sita ya katiba kuhusu maadili na uongozi. Tume ya uwiano na mshikamano wa kitaifa ilisema haiwezi kumshtaki mbunge huyo ambaye kwa muda mrefu alikuwa mwenyekiti wa chama cha wanafunzi wa chuo kikuu cha Nairobi.