Baadhi YA Watoto Huko Kajiado Kukosa Chanjo

Mmoja kati ya watoto wanne katika kaunti ya Kajiado huenda wakakosa chanjo ya kuzuia magonjwa hatari kama vile ukambi, kifua kikuu ,homa ya mapafu, na ugonjwa wa kupooza.

Kulingana na ripoti iliyotolewa na kundi la mashirika ya utoaji misaada yasiyokuwa ya kiserikali hapa nchini , viwango vya utoaji chanjo hapa nchini vilipungua kwa asilimia 82 mwaka wa 2012/2013 hadi asilimia 71 mwaka 2014/2015 huku kaunti za Kajiado na Turkana zikinakili viwango vya chini zaidi vya asilimia 30 .

Mkurugenzi wa kundi hilo Peninah Kamau amesema hali hiyo katika kaunti ya Kajiado imesababishwa na kukithiri kwa hali ya kutojua kusoma na kuandika huku akiongeza kuwa wazazi wengi hawapeleki watoto wao kuchanjwa kwani hawafahamu umuhimu wa chanjo.

Bi. Kamau ambaye alikuwa akiongea kwenye kongamano la umma mjini Kajiado amesema katika eneo hilo kina mama wengi hujifungulia nyumbani na hawapati habari kuhusu jinsi ya kuzuia magonjwa ya utotoni . Amesema chanjo hutolewa bila malipo katika hospitali zote za umma na kuwahimiza kina mama kuhakikisha watoto wao wanachanjwa dhidi ya magonjwa yote ili kupunguza kiwango cha vifo vya watoto katika eneo hilo.