Baadhi Ya Wakaazi Wa Mwingi Watoroka Kwa Kuhofia Uvamizi

Mamia ya wakazi wa Mwingi wanaoishi kwenye mpaka kati ya kaunti za Kitui na Tana River wametoroka makazi yao na kwa sasa wanaishi ndani ya msitu kwa kuhofia kushambuliwa na wachungaji mifugo Wasomali. Wachungaji mifugo hao wanadaiwa kuwauwa watu wawili wiki iliyopita huko Kathungu. Wakazi wa Sosoma, Ndooni na Myuni katika kata ya Ukasi kwenye kaunti ndogo ya Mwingi mashariki wanaishi nje kwenye kambi na watoto wao baada ya majambazi hao kutoka Somalia kuvamia mashamba yao. Kulingana na Simeon Musyimi ambaye ni mkazi wa eneo hilo, wachungaji mifugo wa asili ya Somalia walivamia mashamba yao wakiwa wamejihami kwa bunduki na mapanga na kutishia kumuuwa mtu yeyote atakayewazuia kuwasilisha mifugo wao katika mashamba yao. Mkazi mwingine laeli Musyoka, anasema wanawake na watoto ndio wameathirika pakubwa kwani waliondoka katika makazi yao bila kubeba chochote na akawahimiza maafisa wa usalama huko Kitui kukabiliana na hali hiyo na kutafuta suluhu la kudumu. Aliyekuwa mkurugenzi wa chama cha Wiper Dkt. Gideon Mulyungi ambaye aliwatembelea waathiriwa na kuwapa msaada wa chakula, aliwashtumu maafisa wa usalama huko Ukasi ambao aliwalaumu kwa kuto-hakikisha usalama wakazi ambao wametoroka makazi yao. Alihimiza serikali kutafuta suluhu la kudumu kwa tatizo hilo , badala ya kubakia kimya huku wakazi wakihangaishwa na majambazi hao.