Baa mjini Thika zapunguza saa za kuhudumu wakati wa uchaguzi

Wenye baa mjini Thika pamoja na maafisa wa usalama wamepunguza saa za kuhudumu kwa baa hizo wakati wa uchaguzi ili kuhakikisha kwamba hakutakuwa na wapigaji kura walevi na kwamba idadi kubwa ya wapigaji kura wanajitokeza. Naibu kamishna wa kaunti ndogo ya Thika Tom Anjere amesema kuwa walikubaliana kuwa tarehe 7 mwezi huu baa zitafunguliwa saa nane adhuhuri na kufungwa saa mbili usiku huku zikifunguliwa saa kumi na moja jioni siku ya uchaguzi. Kwenye mkutano na wenye baa katika shule ya watu wasio na uwezo wa kuona ya Thika hapo jana Anjere alisema kuwa maafisa wa usalama wako tayari kulinda usalama kwenye uchaguzi mkuu ujao na kutoa wito kwa wadau wote kushirikiana ili kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki. Afisa mkuu wa polisi katika eneo la Thika magharibi Willy Simba alitoa wito kwa wakazi kudumisha amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi.A�