Askofu Mwarandu Ataka Kuzingatiwa Kwa Mapatano Baada Ya Uamuzi Wa ICC

Mwelekeo ambao Wakenya wapasa kuzingatia kufuatia uamuzi uliotolewa na mahakama ya kimataifa ya ICC ni kuzingatia mapatano kama nchi yenye jamii mbali mbali. Hayo ni kwa mujibu wa askofu Morris Mwarandu wa kanisa la Lords Gathering Centre. Akiongea na shirika la utangazaji nchini-KBC kwa njia ya simu, askofu Mwarandu, alisema mapatano ni muhimu miongoni mwa jamii mbali mbali wakati nchi hii inapoelekea kufanya uchaguzi mkuu mwaka ujao.

Akieleza kuridhika kwake na uamuzi huo, Mwarandu alishangaa kwanini baadhi ya mataifa ya magharibi ikiwemo Marekani hayajawajibikia vitendo vyao vya kikatili nchini Iraq miongoni mwa nchi nyingine.

Akiongea katika kituo kimoja cha runinga hapa nchini wakili wa waathiriwa, Wilfred Nderitu, alisema haki yapaswa kutendewa wateja wake kwa kuwapa makazi na mahitaji mengine ya kimsingi mbali na kuwafidia. Nderitu alisema serikali sharti ihakikishe uchunguzi unafanywa na waliotekelezwa ghasia za baada ya uchaguzi wanashtakiwa. Alimhimiza rais kuzindua hazina ya shilingi bilioni -10 kama alivyoahidi mwaka uliopita.