Amina Mohammed awanusuru wavuvi saba wa Kenya waliofungwa

Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni, Amina Mohammed amefanikiwa kuwanusuru wavuvi saba wa KenyaA�waliokuwa wamezuiliwa na maafisa wa serikali ya Uganda. Hii ni baada ya waziri Mohammed kushauriana na mwenzake wa Uganda Sam Kutesa ambaye alisema kuwa wakenya wengine tisa waliokuwa wakizuiliwa wataachiliwa huru hivi leo. Mawaziri hao wawili wamesema wanatafuta suluhisho la kudumu kuhakikisha raia wa Kenya na Uganda walioko katika kisiwa cha Migingo kilicho na utajiri wa samaki wanaishi kwa amani. Wavuvi hao walikamatwa siku ya ijumaa katika ziwa Victoria wakivua samaki karibu na visiwa vya Riabana na Kalangala huko Uganda, yapata umbali wa kilomita tatu kutoka kisiwa cha Remba kaunti ya Homa Bay. Wabunge kutoka eneo la Nyanza jana waliitaka serikali ichukue hatua kukomesha visa vya kunyanyaswa kwa wakenya katika ziwa Victoria.