Amina Mohamed atarajiwa kukutana na wenyeviti wa mabaraza ya vyuo vikuu vya umma

Waziri wa elimu Amina Mohamed anatarajiwa kukutana na wenyeviti wa mabaraza ya vyuo vikuu vya umma katika juhudi za kutamatisha mgomo wa wahadhiri ambao umelemaza masomo katika vyuo hivyo. Hii ni baada ya wahadhiri kuendelea na mgomo licha ya mahakama ya kusuluhisha mizozo ya ajira kuwaagiza wahadhiri na wahudumu wengine wa vyuo vikuu vya umma waliokuwa wakigoma kurejea kazini. Ijumaa iliyopita, jaji Onesmus Makau aliwaagiza viongozi wa vyama vya wafanyikazi hao kusitisha mgomo huo na kuwashauri wanachama wao kurejea kazini leo. Jaji Makau pia aliagiza chuo kikuu cha Nairobi kuwasilisha pendekezo lake kuhusiana na nyongeza ya mishahara na marupurupu ya wafanyikazi wa vyuo vikuu kwa waziri wa leba, , Ukur Yattani. Pendekezo hilo linatarajiwa kutoa mwongozo wakati wa mashauriano kuhusu mzozo huo. Korti ilikubaliana na wizara za fedha, leba na elimu pamoja na tume ya kuwianisha mishahara na marupurupu ya watumishi wa umma kwamba kushindwa kwa baraza la pamoja la vyuo vikuu kuwasilisha pendekezo hilo kumechelewesha utekelezaji wa mkataba huo.