Aliyekuwa rais wa Korea Kusini Park Geun-hye akosolewa na chama cha upinzani

Rais wa Korea kusini aliyeondolewa mamlakani Park Geun-hye leo amekosolewa vikali kuhusiana na kauli yake kwamba ukweli kuhusiana na kuondolewa kwake mamlakani utadhihirika huku chama kikuu cha upinzani kikiwahimiza viongozi wa mashtaka kutekeleza uchunguzi dhidi yake kwa haraka. Mahakama ya kikatiba ilimwondoa Park mamlakani siku ya Ijumaa ilipodumisha hoja ya bunge ya kumwondoa mamlakani kuhusiana na sakata ya ushawishi ambayo imewaathiri washirika wake wa kisiasa na kibiashara ambapo Park amekanusha kufanya kosa lolote. Park aliondoka kwenye ikulu ya rais jijini Seoul hapo jana jioni na kurejea kwenye makazi yake ya kibinafsi jijini humo kama raia wa kawaida huku akiondolewa kinga yake ya kirais ambayo imemzuia kushtakiwa. Park hajatoa kauli yoyote hadharani tangu uamuzi huo wa mahakama lakini msemaji mmoja alisoma taarifa yake aliporeja nyumbani kwake katika eneo la Gangnam ambapo alielezea maskitiko yake kwa kushindwa kukamilisha kipindi chake cha uongozi.

A�