Aliyehusika Na Ufyatuaji Risasi Kapenguria Ni Afisa Wa Polisi Anayehudumu Katika Kituo Hicho

Polisi wamethibitisha kwamba mtu aliyehusika na shambulizi hatari la ufyatuaji risasi katika kituo cha polisi cha Kapenguria ambako maafisa sita wa polisi walipoteza maisha yao ni afisa wa polisi anayehudumu katika kituo hicho. Kwenye tarifa polisi walisema afisa huyo alirukwa na akili na kuchukua bunduki kutoka eneo la kuwasilisha ripoti kituoni kabla ya kuzuka makabiliano makali ya ufuatulianaji risasi kwa saa kadhaa.
Mshirikishi wa eneo la Rift Valley Wanyama Musiambo alisema maafisa wa usalama walifanya kazi ya ziada kulinda kituo hicho cha polisi na kuhakikisha hakuna mauaji zaidi yanatekelezwa. Afisa huyo wa utawala hata hivyo hakutoa maelezo zaidi kuhusu waliouawa kwani familia za baadhi ya waathiriwa hazijafahamishwa.