Afueni kwa Elachi baada ya mahakama kumrejesha afisini

Spika wa bunge la kaunti ya Nairobi Beatrice Elachi alipata afueni ya muda baada ya kupata agizo la mahakama la kumrejesha kazini muda mfupi baada ya wanachama wa bunge la kaunti ya Nairobi kumwondoa afisini.

Elachi alikuwa amebanduliwa katika wadhifa huo baada ya waakilishi wa wadi 103 kupiga kura kumbandua. Waakilishi wawili wa wadi walipinga hatua hiyo na wengine wawili wakikosa kushiriki kwenye upigaji kura huo. Waakilishi hao wa wadi walimuondoa Elachi kutokana na kile walikitaja kuwa kufedhehesha bunge la kaunti.

Mwakilishi wa wadi wa Waithaka Antony Kiragu ambaye aliwasilisha hoja hiyo alimlaumu Elachi kwa utovu mkubwa wa maadili. Kiragu alisema vitendo vya Elachi vimeleta fedheha na kudhalalisha ofisi ya spika. Awali, Elachi alidai baadhi ya wanachama wa bunge la kaunti walilazimishwa kutia saini rufaa ya kumuondoa Elachi mamlakani. Alikanusha kuwazuia wanachama wa bunge la kaunti hiyo kusafiri.

Aidha alikanusha madai kwamba aliandikia barua tume ya maadili na vita dhidi ya ufisadi kuwachunguza wanachama 19 wa kamati ya Leba kuhusu madai ya ufisadi.Elachi ambaye alikuwa akiongea huko Malindi, alisema aliwaruhusu maafisa wakuu wa bunge hilo kutia saini hati za usafiri za waakilishi wa wadi kutokana na heshima yake kwa maafisa hao.