Afrika Haipaswi Kushinikizwa Kuhusu Miradi: Rais Uhuru

Rais Uhuru Kenyatta amesema mataifa ya kiafrika yana uwezo wa kubaini mahitaji yao ya miundo mbinu. Alisema mataifa ya kiafrika yanafahamu yale yanayohitajika kwa watu wao na hayapaswi kushinikizwa kuhusu miradi ya kutekeleza. Akitaja habari zilizochapishwa kwenye jarida la Economist ambazo zilitaja benki ya dunia ikishtumu mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa hapa nchini, rais Kenyatta alisema nchi hii ndio inafahamu miradi ambayo ni bora kwa raia wake. Akiongea leo katika Ikulu ya Nairobi wakati wa mkutano kuhusu miundo mbinu, rais alisema shtuma sawa na hizo zilielekezwa kwa mataifa ya Asia yenye ustawi mkubwa wa kiuchumi lakini yalipuuza shtuma hizo na sasa yamo miongoni mwa mataifa ambayo chumi zao zinakua haraka zaidi duniani. Kuhusu bandari ya Mombasa, rais Kenyatta alimuagiza mkurugenzi mkuu mpya aliyeteuliwa Cahtherine Mturi, kutokomeza ufisadi bandarini na kuwianisha shughuli za halmashauri ya bandari nchini. Akiongea wakati wa mkutano huo, waziri wa miundo mbinu James Macharia alihakikisha kuwa mpango wa serikali wa ujenzi wa barabara ungali unaendelea. Waziri huyo alisema kufikia mwisho wa mwaka huu ujenzi wa barabara za umbali wa kilomita elfu-7 utakuwa unatekelezwa.