Afisa mmoja wa polisi aliaga dunia huku abiria 31 wakijeruhiwa

Afisa mmoja wa polisi aliaga dunia jana jioni huku abiria 31 wakijeruhiwa vibaya baada ya basi walimokuwa wakisafiria kupata hitilafu za breki na kugonga kizuizi cha barabarani na trela kabla ya kuanguka ndani ya mtaro. Basi hilo la chama cha akiba na mikopo cha Githurai lilikuwa likiwasafirisha abiria kutoka Nairobi hadi Kisumu huku trela hilo likielekea Kericho ajali hiyo ya ana kwa ana ilipotokea kwenye barabara kuu ya Kericho-Sotik kwenye makutano ya Kisumu. Naibu afisa mkuu wa polisi katika kaunti ya Kericho Nathan Sanya alithibitisha kisa hicho akisema kuwa breki za basi hilo zilikumbwa na hitilafu kutoka mjini Kericho ambapo wananchi walijaribu kuweka mawe barabarani ili lisimame lakini ikashindikana huku likigonga kizuizi cha barabarani umbali wa kilomita moja kutoka mjini humo. Sanya alisema kuwa basi hilo liligonga trela lililokuwa likipitia kwenye kizuizi hicho pamoja na afisa mmoja wa polisi aliyekuwa akisimamia kizuizi hicho kabla ya basi hilo kuanguka ndani ya mtaro. Mwili wa afisa huyo ulipelekwa kwenye chumba cha kuhuifdhia maiti cha hospitali ya matibabu maalum ya Kericho huku majeruhi wakipelekwa kwenye hospitali hiyo na ile ya Siloam. Sanya alisema kuwa watafanya uchunguzi kubainisha iwapo basi hilo lina idhini ya kusafiri kwenye barabara hiyo na watachukua hatua zifaazo iwapo litapatikana kwamba lilikuwa limekiuka sheria.