Afisa mmoja mwandamizi wa kaunti ya Nandi ajiyonga

Uchunguzi unaoendelea kuhusu ufujaji wa pesa katika kaunti ya Nandi umegeuka kuwa mkasa baada ya afisa mmoja mwandamizi kujinyonga baada ya kuhusishwa katika kashfa hiyo. Kevin Kemboi, ambaye ni afisa wa huduma za ununuzi alijinyonga na akaacha taarifa inayohusisha ukaguzi wa kimaabaraa wa kifedha ulioagizwa kufanywa na Gavana Stephen Sang wiki mbili zilizopita. Alifanyakazi katika idara ya afya wakati wa uhudumu wa gavana wa zamani Cleophas Lagat kabla ya kuhamishwa katika idara ya ardhi. Maafisa saba waandamizi katika idara ya afya wameagizwa kuchukua likizo ya lazima kuruhusu uchunguzi wa kupotea kwa mamilioni ya pesa. Kulingana na Peter Wambani ambaye ni kamanda wa polisi wa kaunti hiyo, marehemu alimwambia mkewe amtayarishie chai kabla ya kwenda kulala huku akiendelea kutazama mechi ya soka sebuleni. Kaimu katibu wa kaunti Francis Sang alisema marehemu hakuombwa awajibike katika musimamizi mbaya wa fedha uliodaiwa kufanyika kwa vile uchunguzi ulikuwa haujakamilika. Gavana Stephen Sang amewaalika maafisa kutoka ofisi ya mkaguzi mkuu wa mahesabu kufanya ukaguzi wa kubaini pesa hizo zilivyopotea kupitia wizi wakati wa mtangulizi wake Cleophas Lagat na hatua ichukuliwe dhidi ya waliohusika.