Abiria Wanne Wafariki huko Mazeras

Abiria wanne wamefariki leo asubuhi baada ya Basi lililokuwa likisafiri kutoka Nairobi kuelekea Mombasa lilipoacha njia na kutumbukia kwenye bonde huko Mazeras kaunti ya Kilifi. Abiria wengine 21 walipelekwa hospitalini kufuatia ajali hiyo iliyotokea katika eneo lililo hatari kwa ajali. Kulingana na kamanda wa Trafiki eneo la Pwani Emmanuel Okanda, uchunguzi umeanzishwa kufuatia ajali hiyo huku akisema kuwa eneo hilo ni hatari kwa ajali kwenye barabara hiyo kuu ya Mombasa-Nairobi. Hata hivyo, ajali hiyo imetokea siku chache baada ya zaidi ya watu 40 kufariki katika ajali nyingine ya barabarani katika sehemu ya Karai kwenye barabara kuu ya Nakuru-Naivasha. Ajali hiyo mbaya ilihusisha gari aina ya Canter iliyokuwa ikisafirisha bidhaa zinazoshika moto kwa haraka kuelekea nchini Uganda kutoka Mombasa na magari mengine 13.