Wakenya waliokwama Uingereza kurejea nchini

Wakenya waliokwama nchini Uingereza wanatarajiwa kupewa fursa nyingine ya kurejea nchini, baada ya safari nyingine ya ndege kutoka nchini humo kutangazwa.

Balozi wa Kenya nchini humo Manoah Esipisu, alitangaza kuwa safari hiyo kutoka London, imepangiwa  siku ya ijumaa wiki hii.

Safari hiyo ya ndege ya shirika la Kenya Airways, ilipangwa kufuatia mashauriano baina ya serikali za Kenya na Uingereza.

Wakenya  nchini Uingereza wanaotaka kurejea nyumbani wametakiwa kujikatia tikiti kupitia mtandao wa  Kenya Airways.

Na akiongea na wanahabari katika makao makuu ya wizara ya afya, Katibu katika Wizara ya Maswala ya Kigeni Macharia  Kamau alisema kuwa serikali itaendelea kuwasaidia wakenya wanaotaka kurejea nyumbani.


Balozi Macharia kwa niaba ya wizara yake na wahisani wengine alitoa msaada wa vifaa vya kujikinga kwa wizara ya afya kutumika kwenye vita dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.