Bunge lapendekeza uchunguzi zaidi kuhusu kasoro za uagizaji wa sukari

Bunge limependekeza kwamba Idara ya Upelelezi wa Jinai na Tume ya Maadili na Vita Dhidi ya Ufisadi zifanye uchunguzi zaidi wa kasoro zote zinazohusiana na uagizaji sukari hapa  nchini . Kamati ya pamoja ya bunge ya  kilimo, biashara, viwanda na ushirika inataka uchunguzi zaidi dhidi ya waziri wa zamani wa biashara Adan Mohamed na pia ibaini ni kwa nini shirika la ukadiriaji ubora wa bidhaa nchini (KEBS) lilishindwa kufanya uchunguzi wa kina kuhakikisha usalama na ubora wa sukari humu nchini. Taarifa iliyowasilishwa na mwenyekiti mwenza wa kamati hiyo Kanini Kega imependekeza marufuku ya uagizaji wa sukari ambayo haijachakatwa ili ichakatwe zaidi na kuepusha bidhaa hiyo kuuzwa katika soko la hapa nchini.

Wakati huo huo kamati hiyo imependekeza uchunguzi dhidi ya madai ya shughuli zisizo halali kati ya kampuni ya sukari ya SONY na kampuni nyinginezo kwa madai ya kukwepa kulipa ushuru wa takribani shiingi bilioni 2.5. Uchunguzi sawia na huo umependekezwa dhidi ya waagizaji, wauzaji wa jumla na viwanda vya kusaga sukari vinavyojihusisha na sukari iliyoharibika kuchunguzwa kabla ya kushtakiwa kwa ukiukaji wa sheria ya vyakula, dawa , kemikali na sheria ya afya ya umma.