Wakenya wahisi mwaka wa 2017 ulikuwa mgumu sana

Wengi wa wakenya wanahisi kuwa mwaka 2017 ni mwaka mgumu zaidi ukilinganishwa na mwaka 2016. Kwenye utafiti uliofanywa kampuni ya utafiti ya Trends and Insights For Africa TIFA asilimia 75 ya wakenya wanahisi kuwa mwaka 2017 ni mwaka mbaya zaidi huku gharama ya juu ya maisha ikitajwa kuwa changamoto kuu. Hata hivyo huku joto za kisiasa zikipungua wengi wanasubiri mwaka mpya wakiwa na matumaini kuwa mwaka 2018 utakuwa afadhali. Kulingana na utafiti huo changamoto kuu iliyoshuhudiwa mwaka n 2017 ilikuwa ni gharama ya juu ya maisha kwa asilimia 64 na kufuatiwa na taharuki ya kisiasa kwa asilimia 52 . Ukosefu wa ajira uliorodheshwa katika nafasi ya tatu kwa asilimia 25. Afisa mkuu mtendaji wa kampuni hiyo Maggie Ireri amesema msimu mrefu wa uchaguzi pamoja na ukame uliathiri vibaya uchumi hali iliyosababisha mfumo wa bei za bidhaa na kupunguza matumaini ya kupatikana kwa nafasi za ajira. Swala jingine lililowatia wakenya wengi kiwewe mwaka 2017 ni mgomo wa madaktari uliodumu kwa siku 100 na kulemaza utoaji huduma katika hospitali za umma huku makumi ya watu wakifariki. Utafiti huo ulilenga wakenya wa umri wa zaidi ya miaka 18 na huku watu 1,005 wanaoishi katika maeneo ya mijini na mashambani wakihojiwa.