Hospitali ya rufaa ya Chuo Kikuu cha kenyatta yafunguliwa rasmi na Rais Kenyatta

Rais Uhuru Kenyatta Jumatano  aliongoza  hafla ya kufunguliwa rasmi kwa hospitali ya mafunzo na rufaa ya Chuo kikuu cha Kenyatta.

Katika hafla hiyo, Rais alimpongeza mwenyekiti wa bodi ya hospitali hiyo Prof. Olive Mugenda kwa kujitolea kwake kuhakikisha maono ya kuwepo kwa hospitali hiyo yameafikiwa.

Alisema kufunguliwa kwa hospitali hiyo ni hatua kubwa kwa nchi hii Kwani tayari hospitali hiyo ya rufaa imetia saini mkataba wa maelewano na Chuo Kikuu cha Manchester wa kubuniwa kwa kituo cha utafiti wa saratani na kutoa mafunzo kwa wafanyikazi wake wote.

Alipongeza uwezo wa hospitali hiyo wa kugundua mapema na kutibu ugonjwa wa saratani na figo na hivyo kusaidia nchi hii kuokoa fedha.

Rais Uhuru Kenyatta alifanya ziara katika hospitali hiyo kabla ya kuweka jiwe la msingi.

Hospitali hiyo yenye vitanda   650 ina vifaa vya kisasa vitakavyotumiwa kutoa huduma mbali mbali za matibabu.

Hospitali hiyo ya kiwango cha Level 6, itakuwa chini ya usimamizi wa wizara ya afya.

Hospitali hiyo ambayo iko katika kaunti ya Kiambu inatarajiwa kupunguza msongamano wa wagonjwa wanaotafuta huduma katika hospitali kuu ya kitaifa ya Kenyatta na kuleta huduma karibu na wananchi.

Dkt. Alex Muturi  ambaye ni afisa mkuu wa oparesheni kwenye hospitali hiyo alikuwa na haya ya kusema.

Dkt. Muturi aliongeza kwamba hatua zimechukuliwa kuhakikisha sheria zilizopendekezwa na wizara ya afya ili kuhakikisha upo  usalama wa wahudumu pamoja na wagonjwa zinazingatiwa.

Hospitali hiyo ilijengwa kwa gharama ya shilingi bilioni nane.

Ufunguzi wa hospitali hiyo unaambatana na ajenda nne kuu za rais Uhuru Kenyatta kuhakikisha huduma za afya kwa wote.

Hospitali hiyo ya rufaa ya Kenyatta itatoha huduma za matibabu ya saratani na hivyo kupunguza muda mrefu ambao wagonjwa wa saratani husubiri kupata matibabu humu nchini.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *