Categories
Michezo

uchaguzi wa matawi ya Fkf waendelea mbele ilivyopangwa

Uchaguzi wa matawi ya Fkf umeanza vyema mapema leo katika kaunti tofauti huku hitilafu kadhaa zikiripotiwa.

Kwa mjibu wa mwenyekiti wa Bodi ya uchaguzi huo Bi Kentice Tikolo wamelazimika kuhamisha ukumbi wa kupigia kura kwa tawi la Nairobi West kutoka Pumwani hadi ligi Ndogo.

Uchaguzi huo unaandaliwa katika kaunti 17 baada ya ule wa kaunti ya Garisa kusimamishwa kufuatia agizo la mahakama kutokana na mmoja wa wagombezi kuwasilisha kesi katika mahakama kuu.

Uchaguzi wa leo unatoa fursa kwa ule wa kitaifa tarehe 17 mwezi ujao ambapo wagombeaji watano  wa urais na wawaniaji wa viti vya Nec watabaini hatima yao.

 

Categories
Vipindi

Marwa amesisitiza fedha billion 8.5 zilizotolewa na serikali kwa wazee na walemavu zitawifikia

Katibu wa Huduma za Jamii Nelson Marwa amesisitiza fedha billion 8.5 zilizotolewa na serikali kwa wazee na walemavu zitawifikia hivi karibuni.

Akizungumza na Wanahabari wa Radio Taifa Bernard Maranga na Cynthia Anyango, Marwa aliongeza kuwa wizara ya Leba itakabiliana na wale wanaotumia walemavu au watoto kujinufaisha.

https://podcasts.kbc.co.ke/wp-content/uploads/2020/04/PS-SOCIAL-PROTECTION-NELSON-MARWA-RADIO-TAIFA-23RD-APRIL-2020.mp3
Categories
Burudani

Marehemu Madilu System mmoja wa wanamuziki bora wa mtindo wa Rhumba

Jean De Dieu Maieke au Madilu Bialu System anavyojulikana na wapenzi wa muziki wa Rhumba anaendelea kusifiwa miaka 13 baada ya kuaga dunia. Hili linadhihirika wazi kutokana na weledi wake katika kutunga na kuimba nyimbo za rhumba kwa sauti ya kipekee.

Madilu alizaliwa mwaka 1952 tarehe 25 mwezi mei katika eneo la Leopoldville, Belgian Congo ambalo kwa sasa linajulikana kama Kinshasa na nchi pia ilibadili jina na kuitwa Congo. Alikuwa mmoja wa waimbaji katika bendi ya TPOK Jazz iliyodumu miaka ya sitini hadi themanini. 

Akiwa kijana mdogo Mailu alianza kuomba kwenye kikundi cha Ochestre Symba, kisha akaingia Ochestre Bambula chini ya uongozi wa Papa Noel na katika Festival des Maquisards iliyokuwa ikiongozwa na Sam Mangwana. 

Madilu alipata umaarufu nchini Congo na kimataifa wakati alijiunga na Franco Luanzo Luambo Makiadi ambaye wengi wanamwita baba ya muziki wa Rhumba nchini Congo. Franco ndiye alimpa jina la “Madilu System” na likabakia kuwa lake kabisa.

 

Wimbo wa kwanza ambao Madilu aliuimba akiwa TPOK Jazz ya Franco ni ‘Mamou’ ambao ulifikia kilele mwaka 1984 na hadi sasa unapendwa. Katika wimbo huo wanawake wawili wanalaumiana kwa mienendo yao isiyofaa ya kutokuwa waaminifu katika ndoa na uasherati.

Ndoa ya mmoja inaonekana kuingia doa kwa sababu ya tabia yake na anamlaumu mwenzake kwamba yeye ndiye amemsema kwa mumewe na kusababisha ndoa yake kuharibika.

Mamou ni jina la mwanamke.

Baada ya wimbo Mamou, Madilu aliandika na kuimba wimbo uitwao ‘pesa position’ akiwa bado TPOK jazz alafu akaimba ‘Mario’ na jibu la wimbo Mario mwaka 1985. Aliimba nyimbo nyingi tu akiwa katika kundi hilo lililokuwa likiongozwa na Franco.

Kufuatia kifo cha Franco mwaka 1989, kundi la TPOK Jazz liliacha kuimba kwa mwaka mzima kabla ya kurejelea kazi Madilu akiwa mmoja wa viongozi.

Alifanya kazi na kikosi hicho kwa muda kabla ya kuanza kuimba peke yake na akahamia mjini Paris nchini Ufaransa na baadaye akahamia Geneva nchini Uswizi. Muda huo wote bado alikuwa na mashabiki wengi mjini Kinshasa nchini Congo.

Mwanzo wa mwaka 2007 Madilu alirejea nyumbani kwa ajili ya kutengeneza video za nyimbo zake. Ilipofika tarehe 10 mwezi Agosti mwaka 2007 alizirai akapelekwa katika hospitali ya chuo kikuu cha Kinshasa ambapo aliaga dunia kesho yake.

 

Wimbo wake ambao pia unapenda na vizazi vyote ni ‘colonisation’ ambao unahusu bwana mmoja kwa jina Philipo. Philipo anaonekana kuwa na jicho la nje na mke wake analilia Mungu aje amsaidie kabla hajafa kwa sababu ya shida za mume wake.

 

Categories
Habari

Washukiwa wa lile shambulizi la Westage wafikishwa mahakamani Jijini Nairobi

Washukiwa watatu wa shambulizi la kigaidi la mwaka wa  2013 katika jumba la Westgate walifikishwa katika mahakama moja ya Nairobi.

Hata hivyo kesi hiyo yao iliahirishwa hadi tarehe 5 mwezi Octoba. Walifika mbele ya hakimu wa Nairobu  Francis Andayi.

Walikabiliwa na mashtaka matatu yaliyojumuisha kuhusika na shambulizi dhidi ya jumba la Westgate, kusaidia kundi la kigaidi na kuwa nchini kinyume cha sheria.

Wakati wa kikao cha mahakama, mshukiwa mmoja  Mohammed Ahmed Abdi aliiambia mahakama kuwa alikuwa akihitaji blanketi zaidi kwa vile kulikuwa na baridi nyingi gerezani.

Mshukiwa wa pili Liban Abdullahi alilalamikia lishe duni huku mshukiwa wa tatu Hussein Hassan Mustafa akilalamikia kuto-ona vizuri.

Andayi alitoa wito kwa maafisa katika idara ya mahakama kushughulikia maswala hayo na kuwasilisha ripoti mahakamani katika siku kumi zijazo.

Wakati wa shambulizi dhidi ya jumba la Westgate Septemba mwaka wa 2013, wavamizi waliwafyatulia risasi wateja na watu waliokuwa katika jumba hilo na kuwaua watu wapatao  67 na kuwajeruhi wengine 150.

Categories
Burudani

The Rock avunja lango la makazi yake, kulikoni?

Muigizaji mmarekani Dwayne Johnson almaarufu “The Rock” alivunja lango la makazi yake Ijumaa asubuhi kulingana na saa za nchi hiyo.  Kupitia ukurasa wake wa facebook Dwayne alielezea kwamba lango hilo la makazi yake hufungwa na kufunguliwa kwa kutumia nguvu za umeme.

Lango alilolivunja The Rock

 

Eneo analoishi Dwayne limekuwa bila nguvu za umeme kwa sababu ya mvua nyingi ambayo inaendelea kunyesha.

The rock alisema hakuwa na la kufanya ila kuvunja lango hilo kwa mikono yake ili awahi kazini maanake wengi wanaofanya kazi naye walikuwa wakimsubiri.

Alivyoelezea masaibu yake kupitia Facebook

 

Mafundi wa kutengeneza lango hilo hawakuamini walichokiona walipowasili saa moja baadaye, kwamba Dwayne ana nguvu za kuweza kuvunja lango hilo.

Dwayne ni mmoja wa waigizaji wakuu katika kipindi cha mieleka cha WWE ambacho miaka ya nyuma kilikuwa kikionyeshwa kwenye Runinga ya KBC.

The Rock alikuwa akipendwa sana na mashabiki wa kipindi hicho kwani haikuwa rahisi kwake kushindwa kwenye pigano lolote na kwa maneno ambayo alikuwa akitumia kama kitambulisho chake akiingia uwanjani, ambayo ni “Do you smell what the Rock is cooking?” Tafsiri ya moja kwa moja ni “je unanusa anachokipika the rock?”

Nia ilikuwa kuonyesha kwamba hungejua mipango yake katika pigano.

Dwayne alijulikana kwanza kwa sababu ya maonyesho ya mieleka ambapo alikaa kwa miaka 8 kisha akaacha na kuingilia uigizaji katika filamu.

 

Categories
Habari

Kampuni ya Kenya Morgage Refinance yaidhinishwa kufadhili ununuzi wa nyumba nchini

Benki kuu ya  Kenya imeidhinisha kampuni ya Kenya Mortgage Refinance kuwa kampuni ya kwanza ya kutoa mikopo ya kufadhili ununuzi wa nyumba nchini.

Kwenye taarifa, benki kuu ya Kenya ilisema kuwa kampuni hiyo itawezesha au kufanikisha kutoa fedha kwa muda mrefu kwa kampuni za kimsingi za kukopesha pesa za kununua nyumba.

Kampuni za kimsingi za kukopesha pesa za kununua nyumba ni benki za biashara, kampuni za kufadhili ununuzi wa nyumba na vyama vya ushirika vya akiba na mikopo.

Kutoa leseni kwa kampuni hiyo kutahakikisha na kuzidisha mikopo ya gharama nafuu ya kununua nyumba kwa wananchi.

Wenye hisa katika kampuni hiyo ni serikali ya  Kenya na kampuni za kimsingi za kutoa mikopo.

Kampuni hiyo inatarajiwa kupiga jeki ajenda nne kuu za serikali kwa kutoa nyumba za gharama nafuu kwa idadi kubwa ya wakenya.

Leseni hiyo imetolewa kuambatana na sheria za benki kuu ya Kenya za utoaji pesa za ufadhili wa ununuzi wa nyumba za mwaka wa  2019 baada ya kampuni hiyo kitimiza mahitaji ya kutoa leseni.

Kampuni hiyo ilisajiliwa tarehe 19 mwezi Aprili mwaka wa  2018 chini ya sheria za kampuni ya mwaka wa  2015 kama kampuni ya umma.

 

Categories
Habari

Agizo la kusitishwa kwa shughuli katika kaunti lafutiliwa mbali

Mwenyekiti wa baraza la magavana Wycliffe Oparanya ameondolea mbali lile agizo la kusitishwa kwa shughuli kwenye maeneo ya kaunti.

Akiongea wakati wa hotuba ya gavana wa Bungoma katika bustani ya chuo kikuu cha Kibabi, Oparanya alisema agizo hilo limeondolewa baada ya bunge la seneti kuafikiana kuhusu mfumo wa ugavi wa mapato kwa serikali za kaunti.

Oparanya alimshukuru rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga kwa hatua yao ya kuingilia kati na kusaidia katika utatuzi wa mzozo huo.

Akiongea,waziri wa ugatuzi Eugene Wamalwa aliyehudhuria halfa hiyo pia alimpongeza Rais kwa kuahidi kuongeza shilingi bilioni 50 kwa mgao wa fedha za kaunti mwaka ujao,akisema hatua hiyo itachangia pakubwa kudumisha ugatuzi nchini.

Pia alitoa wito wa ungwaji mikono mchakato wa BBI unaopendekeza fedha zaidi kutengewa serikali za kaunti.

Baraza la magavana lilikuwa limetangaza kusitishwa kwa huduma zinazotolewa na serikali za kaunti kutokana na uhaba wa kifedha uliosababishwa na mzozo kwenye seneti kuhusu mfumo wa ugavi wa mapato.      

Bunge la Senate lilikuwa limeshindwa mara 10 kupiga kura kuhusu mfumo wa mtu mmoja shilingi moja kura moja.

Bunge hilo lilipiga kura hiyo Alhamisi alasiri  huku maseneta wote waliochaguliwa waliokuwa bungeni wakiunga mkono.

Kamati ya wanachama 12 iliyopewa jukumu la kuleta maafikiano kuhusu mfumo huo uliokuwa ukizua utata ilikuwa imeafikia makubaliano awali.

 

Categories
Habari

Noordin Haji azindua jopo la kuchunguza kashfa za ufisadi katika halmashauri ya KEMSA

Mkurugenzi wa mashtaka ya umma  Noordin Haji amezindua jopo la viongozi wa mashtaka kuchunguza na kutathmini ile kashfa ya shilingi bilioni 7.8 inayokumbwa halmashauri ya usambazaji wa vifaa vya matibabu ya Kemsa.

Haji alizindua jopo hilo baada ya kupokea faili ya uchunguzi kutoka kwa tume ya kukabuliana na ufisadi nchini EACC.

Kwenye taarifa, Haji alisema jopo hilo linatarajiwa kukamilisha ripoti yake katika muda wa siku 14 zijazo.

Kulingana na tume ya EACC,uchunguzi wake umeabaini kuwa maafisa wa Kemsa walikiuka sheria za ununuzi wa bidha za umma na ile ya usimamizi wa fedha za umma.

Kwenye kwenye taarifa afisa mkuu wa tume ya EACC Twalib Mbarak,tume hiyo imependekeza mashtaka ya uhalifu dhidi ya wahusika.

Tume ya EACC ilikuwa ikichunguza jinsi zabuni za uuzaji wa vifaa vya kujikinga na maambukizi ya virusi vya COVID-19 vya thamani ya mabilioni ya pesa,zilivyotolewa.

Zabuni hizo zinasemekana kutolewa kwa kampuni zinazohusishwa na wanasiasa na wafanyibiashara wenye ushawishi mkubwa ambao baadhi yao hawakuwasilisha bidha hizo kwa Kemsa.

Miongoni mwa maafisa wakuu waliohojiwa kufikia sasa ni pamoja na mwenyekiti wa bodi ya  KEMSA Kembi Gitura, wanachama wa bodi hiyo na baadhi ya wafanyikazi wanaohusika na utaoji wa zabuni.

Uchunguzi huo ulizinduliwa kufuatia agizo la rais Uhuru Kenyatta ambaye aliamuru ripoti hiyo kuwa tayari mwezi huu baada ya wachunguzi kupewa majuma mawili kuitayarisha.

Categories
Burudani

Siku nitakufa mnizike mara moja! Akothee

Mwanamuziki Esther Akoth Kokeyo maarufu kama Akothee amesema kwamba siku ambayo ataiaga dunia anataka azikwe mara moja.

Akothee alikuwa akizungumzia matatizo ambayo mamake mzazi amepitia kwa muda wa mwezi mmoja akisubiri mwili wa mkaza mwanawe usafirishwe kutoka Uganda hadi nchini Kenya kwa mazishi.

Wifi huyo wa Akothee kwa jina Sarah Anne Atieno Kokeyo aliaga dunia tarehe ishirini mwezi wa nane mwaka huu akipokea matibabu katika hospitali ya mtakatifu Benedict mjini Kampala nchini Uganda.

Vikwazo vya usafiri kwa lengo la kuzuia kusambaa kwa virusi vya Korona vilisababisha iwe vigumu kuuwasilisha mwili huo nchini Kenya mara moja kwa mazishi.

Akothee anasema hataki mamake asononeke kwa muda mrefu ati kwa sababu ameaga dunia.

Mwanamuziki huyo pia aliwasuta watu ambao hata sasa wanamtumia jumbe za kuomba michango kwa ajili ya mazishi ya wapendwa wao na yeye hakuna hata ambaye amejitolea kwenda naye kwa mazishi ya wifi yake.

 

Marehemu Sarah Kokeyo atazikwa tarehe 21 mwezi huu wa Septemba mwaka huu nyumbani alikozaliwa Akothee eneo la Kanyasrega kaunti ya Migori.

Categories
Burudani

Hila za mitandaoni, kuigizwa kwa watu mashuhuri kama vile Esther Arunga

Jana jioni wakenya walichangamkia swala la mwanahabari shupavu wa lugha ya kiingereza Esther Arunga kurejea nyumbani hasa kwenye mtandao wa Twitter. Wengi hawakujua kwamba walikuwa wanahadaiwa tu.

Akaunti moja ambayo inasemekana kufunguliwa mwanzo wa mwaka huu ilibadili jina na kujiita Esther Arunga na kuomba wakenya msamaha na kwamba angependa kurejea nyumbani.

Wakenya wengi walionekana kumpa Esther wa kuigiza msamaha na kumkaribiisha nyumbani. Wengine walionekana kuwa wagumu na kuendelea kumhukumu kwa vitendo vyake vya siku zulizopita.

Akaunti hiyo inasemekana kutumika wakati fulani kuiga mchekeshaji wa redio Felix Odiwuor au ukipenda Jalang’o.

Esther Arunga alikuwa mtangazaji wa runinga ambaye alikuwa akileta habari na mahojiano kwa lugha ya kiingereza. Kitaaluma Esther Arunga amesomea sheria na kwa sasa anaishi nchini Australia.

Mwaka 2009 alijiunga na kanisa la “finger of God” ambalo lilianzishwa na Bwana Joseph Hellon ambaye wana ukoo naye.

Alichumbiwa na Wilson Malaba ambaye alikuwa mzee wa kanisa ila mwaka 2010 akavunja uhusiano naye, akahama kutoka nyumbani kwao akaenda kuishi kwenye nyumba moja iliyokuwa ikimilikiiwa na kanisa. Esther aliwekea wazazi wake lawama kwamba walikuwa wakimlazimisha aolewe na mwanasiasa fulani. 

Esther alijiuzulu kazi yake ya utangazaji jambo ambalo lilionekana kuwakera mashabiki wake.

Wakati fulani Esther, mwanzilishi wa kanisa la finger of God na watu wengine walitiwa mbaroni kwa kuendesha shirika ambalo halikuwa limesajiliwa rasmi.

Baada ya siku tatu Esther aliachiliwa huru na hapo ndipo alishtaki wazazi wake, daktari wake wa matatizo ya kiakili, mwanasheria mkuu na idara ya polisi kwa kile alichokitaja kuwa kukamatwa na kudhulumiwa. 

Esther na mume wake Quincy Timberlake walihamia Australia ambapo Esther alikwenda akajisajili kama wakili na akakubaliwa kuhudumu na mahakama ya juu ya New South Wales.

Mtoto wao mkubwa aliaga dunia mwaka 2014 nyumbani kwa njia ambayo haikueleweka jambo ambalo lilipelekea Quincy kukamatwa na kushtakiwa mwezi wa tisa mwaka 2014.  Esther naye alikamatwa baada ya kubadili ushuhuda wake kwenye kesi ya kuaga kwa mwanao.

Esther alikiri kwamba Quincy aliumiza mtoto wao kwa kumpiga kwenye tumbo wakati akimwombea apone. Esther alilaumiwa kwa kuwa mshirika kwenye mauaji ya mtoto wao kwa kuficha ukweli ila aliachiliwa kwa dhamana. Binti huyo alibadili jina na kujiita “Chryslertte Provydence Timberlake”.

Tangu mwaka 2016 hakuna habari zozote ambazo zimesikika kuhusu wawili hao hadi hapo jana ambapo walaghai waliamua kuchangamsha wakenya.

Kwa sasa usimamizi wa mtandao wa twitter unaziweka alama akaunti za watu mashuhuri ili kuzibainisha na zile za walaghai wanaotumia tu majina ya watu mashuhuri.